migomba 2Katika miaka iliyopita, mikoa inayolima migomba kama vile Kagera na Kilimanjaro, zao hili lilikuwa likistawi vizuri sana na mikungu ya ndizi ilikuwa mikubwa na mizuri kutokana na udongo kuwa na rutuba ya kutosha.
Ardhi katika kipindi hicho ilikuwa tele na rahisi kupata maeneo mapya yenye mboji hasa yale yaliyokuwa yakipatikana baada ya wakulima kukata miti na kuotesha migomba. Baada ya kipindi hicho, kilimo cha migomba kilianza kuwa na matatizo makubwa kama yafuatayo;
Rutuba ya udongo kupungua
Hii inatokana na kustawisha migomba katika shamba lilelile mwaka hadi mwaka bila kuongeza mbolea ya aina yoyote, hasa mboji na samadi. Mvua zinazonyesha huondoa udongoni vyakula vya migomba. Upandaji wa aina mbalimbali za mimea katika shamba moja huondoa aina mbalimbali za vyakula vya migomba.
Mabadiliko ya hali ya hewa
Migomba huhitaji sana maji. Kwa bahati mbaya siku hizi mvua hazinyeshi kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. Hii ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na uteketezaji wa misitu ya asili na misitu ya kupanda. Matokeo yake ni migomba kukosa maji ya kutosha. Mbali na tatizo hili, upepo mkali na mvua za mawe huharibu mashamba mengi ya migomba.
Upungufu wa wafanyakazi
Huko nyuma, katika baadhi ya mikoa, palikuwa na wakulima ambao walianzisha mashamba ya migomba na kuyatunza kwa msaada wa vibarua. Kwa bahati mbaya katika miaka ya hivi karibuni vibarua wa aina hii hawapatikani. Matokeo yake ni kuwa wenye mashamba makubwa kiasi wamepungukiwa nguvu kazi. Hii imesababisha sehemu kubwa ya mashamba yao kutokutunzwa vizuri.
Watu wenye uwezo kutokufanya kazi za shamba
Kuna vijana wengi wanaomaliza elimu ya msingi kila mwaka, huku taifa na wazazi wao wanategemea warudipo majumbani wasaidie wazazi wao kwa kushiriki kutunza mashamba yao. Lakini hii sivyo ilivyo kwa siku hizi, nguvu yao ya kazi za shamba imepungua sana na wengi wa wazee hao wamezeeka sana na afya zao sio nzuri. Matokeo yake ni kuwa familia nyingi zimezungukwa na mashamba ya migomba na kahawa yasiyotoa tena mavuno mazuri.
Wanyama waharibifu
Katika baadhi ya vijiji lipo tatizo la wanyama waharibifu mfano nguruwe (ambao huharibu mashina ya migomba) nyani na tumbili ambao hula matunda ya migomba. Tatizo hili ni kubwa katika sehemu mbalimbali za nchi yetu zinazostawisha migomba kwa wingi.
Kutojua kanuni za kilimo cha kisasa
Wakulima walio wengi, hawajui kanuni za kilimo cha zao la migomba, yaani kulima kwa kitaalamu. Kwa mfano wakulima wengi hawajui namna ya kudhibiti vifukusi vya migomba na magonjwa mengine.
Upungufu wa ardhi inayofaa
Siyo kila sehemu ya ardhi inaweza kustawisha aina muhimu za migomba kwa wingi na kwa urahisi. Sehemu nyingi zinazofaa sana kwa kustawisha migomba ni zile ambazo kwa sasa zinastawisha zao hilo. Kwa bahati mbaya au nzuri, sehemu hizo zina watu wengi mno kwa kila eneo la kilometa ya ardhi na tayari kuna upungufu wa ardhi kwa ajili ya upanuzi wa kilimo. Hii ina maana kwamba uzalishaji wa ndizi nyingi zaidi hauwezi kufikiwa kwa kuongeza maeneo ya migomba (maana ardhi haipo) bali kwa kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Kutokuwepo kwa mifumo mizuri ya uuzaji wa ndizi
Hakuna utaratibu maalumu wa kuuza ndizi kama ilivyo kwa mazao mengine kama vile kahawa, tumbaku, pareto, nafaka na kadhalika yanayoshulikiwa na vyama vya ushirika na bodi za mazao.
Usafirishaji mbaya
Tatizo lingine linalokabili kilimo cha migomba ni usafiri mbaya katika baadhi ya vijiji na wilaya hasa vilivyo mbali na miji ambayo ndiyo yenye wanunuzi wengi.
Kupuuzwa kwa utafiti
Utafiti kuhusu mbinu mbalimbali za kustawisha migomba pia ulidharauliwa kwa muda mrefu ukilinganisha na mazao makuu mengine, hasa yale yanayojulikana kama mazao ya biashara. Hii imesababisha zao hili libaki nyuma kiutafiti na matokeo yake ni kuendelea kukumbwa na matatizo ambayo yangetatuliwa mapema.
No comments